Hanang
Women Counseling and Development Association (HAWOCODA) ni asasi isiyokuwa ya
kiserikali ambayo ni ya kujitolea, inayojitegemea na ni asasi ambayo si ya
kibiashara. Ilianzishwa mwaka 1992 na kusajiliwa rasmi mwaka 1994 chini wizara
ya maendeleo ya jamii kwa nambari ya usajili SO.8263, ikiwa na lengo kuu la kutoa huduma za msaada wa Sheria kwa
watu wote wasiojiweza waishio wilaya ya Hanang’ wakiwemo; watu maskini,
wanawake, watoto, walemavu na watu waishio na virusi vya UKIMWI. Mbali na lengo
hilo HAWOCODA pia imeanzishwa kwa madhumuni ya kueneza elimu ya Sheria kwa
kuandika na kutoa machapisho mbalimbali ya Sheria. Hii ni moja ya njia za
kuhakikisha kuwa wana Hanang wote wanapata elimu ya msingi inayohusiana na
masuala ya Sheria hasa katika kujua haki zao ili kujenga jamii ambayo
inaheshimu Utawala wa Sheria, Utawala Bora, na kuheshimu, kulinda, na
kutekeleza misingi ya Haki za Binadamu.
Kazi
za HAWOCODA
HAWOCODA
inafanya kazi za Sheria zikiwemo; uwakilishi Mahakamani, na usuluhishi wa
migogoro kwa kuzingatia maslahi ya watu maskini. Pia HAWOCODA inafanya kazi ya
kutoa elimu ya Sheria kwa jamii ili kuongeza uelewa wa masuala ya Sheria na
Haki za Binaadamu kwa kupitia semina, makongamano, midahalo na mijadala
inayohusiana na masuala ya Sheria ili kuwawezesha watu kutoka sehemu tofauti
kujadili sera za Sheria na kimaendeleo. HAWOCODA pia inaandaa mikutano ya
kitaalamu kwa ajili ya kutoa mafunzo kutoka sekta tofauti katika jamii ya
Hanang.
Shughuli
za HAWOCODA
Malengo
ya HAWOCODA yanatimizwa kwa kutekeleza shughuli zifuatazo:-
1. Ushauri wa Sheria;
2. Mafunzo ya Wasaidizi wa Sheria;
3. Mafunzo ya Haki za
Binaadamu;
4. Utoaji wa Haki;
5. Usambazaji wa Majarida,
Vitabu na Vipeperushi;
Dira
ya HAWOCODA
Azma
ya HAWOCODA ni kuhakikisha kwamba kila mwana Hanang, hasa watu maskini,
wanawake, watoto, watu wenye ulemavu na makundi yote katika jamii wanaelewa
vizuri haki zao za msingi za Sheria na kanuni za Haki za Binaadamu na pia
waweze kuzidai ili kujenga jamii iliyojengwa kwenye msingi ya utawala wa Sheria,
utawala bora na kuheshimu misingi ya haki za binaadamu.
Dhamira
ya HAWOCODA
HAWOCODA
imekusudia kuongeza uelewa wa jamii juu ya haki zao na wajibu kwa kutoa elimu
ya Sheria na Haki za Binaadamu, utafiti wa maswala ya Sheria, kuendesha semina,
warsha, mikutano, na kutoa ushauri wa msaada wa Sheria.
Wafanyakazi
wa HAWOCODA
Kwa
sasa HAWOCODA ina wafanyakazi na wahudumu wa kada mbali mbali wapatao 29 kutoka
katika kata 11 za wilaya ya Hanang.
Maadili
ya HAWOCODA
Watu
wote wanaoshiriki katika shughuli za HAWOCODA ni lazima wawe ni watu wenye
dhamira nzuri kwa watu wote katika masuala yote yanayohusiana na HAWOCODA, na
hawaruhusiwi kutumia huduma pamoja na jina la HAWOCODA kwa ajili ya maslahi yao
binafsi, kisaisa, kidini, kikabila, au jambo lolote ambalo liko nje ya malengo
ya HAWOCODA.
Anwani
Unaweza
kuwasiliana na HAWOCODA kwa anuani ifuatayo:-
Head Office (Katesh)
Hanang’ Women Counselling and Development Association (HAWOCODA)
S.L.P. 3, Katesh - Hanang.
Simu: +255 (0) 784 739 773 – Gidamis Shahanga (M/kiti wa Bodi)
+255 (0) 784 779 096 – Mary Gitagno (Mratibu)
Ofisi ya Balang’dalalu:
Hanang’ Women Counselling and Development Association (HAWOCODA)
S.L.P. 3, Katesh - Hanang.
Simu: +255 (0) 686 209 304 – Christopher Digay
Barua Pepe: hawocoda@yahoo.com
Maelezo
ya Jumla
Moja
ya lengo kuu la HAWOCODA ni kutoa msaada wa Sheria bila ya malipo. Hivyo, kazi
hii ilianza kutekelezwa mara tu baada ya kuanzishwa kwa HAWOCODA kwa kutumia wasaidizi
wa Sheria waliopata elimu ya msingi ya Sheria mbalimbali za nchi na Katiba ya
jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Idadi ya watu wenye kuhitaji
huduma hii ilikuwa ikiongezeka kila kukicha, na hivyo uhaba wa huduma hizo
ulianza kuonekana. Baada ya kuongezeka kwa idadi ya watu wa Hanang na walio
wengi kuanza kupata uelewa juu ya haki zao na hivyo kujitokeza kwa wingi kutaka
huduma. Hapo ndipo HAWOCODA ilipoanza kutafuta njia mbadala ya kukidhi haja
hiyo na kuona kuwa upo umuhimu wa kupanua wigo wa huduma za msaada wa Sheria mijini
na vijijini. Hivyo basi HAWOCODA ilibuni utaratibu wa kuweka Wasaidizi wa Sheria
katika sehemu zote za Hanang ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo.
Hivyo
mnamo mwaka 2015 HAWOCODA ilianzisha rasmi mpango huo. Mpaka sasa, HAWOCODA imeweza
kuwaajiri Wasaidizi wa Sheria wasiopunguwa 25 ambao wamesambazwa katika kata mbalimbali
za wilaya ya Hanang. Wasaidizi hao wamepatiwa elimu ya msingi inayohusiana na
masuala ya Sheria pamoja na kupata maelekezo kutoka kwa maafisa mipango wetu
juu ya utoaji wa msaada wa Sheria.
Licha
ya hayo HAWOCODA pia imeona iko haja ya kutayarishia Wasaidizi hawa muongozo
ambao utakuwa unawaongoza katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi. Umuhimu wa
muongozo huu ni kuwa umejaribu kugusia nyanja zote ambazo ni muhimu katika
kuhakikisha Utawala wa Sheria unakuwepo wilayani ikiwemo; Katiba ya Jamhuri wa
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na misingi mikuu na kanuni muhimu
zilizomo ndani yake kama vile Utawala wa Sheria, Uhuru wa Mahakama, Haki na
wajibu wa Binaadamu, Utawala Bora, Mihimili mikuu ya Serikali pamoja na kazi
zake, Sheria za ajira na mahusiano kazini, Sheria za Ardhi, Sheria za mwenendo
wa Makosa ya Jinai na Makosa ya Madai, Sheria za Tawala za Mikoa, Sheria za
mazingira, mikaaba ya kimataifa ya haki za wanawake, tamko la kimataifa la haki
za binadamu, mkataba wa kimataifa wa kupinga aina zote za ubaguzi dhidi ya
wanawake, na Sheria nyinginezo za nchi.
Katika
kuhakikisha wasaidizi wa Sheria wanafanyakazi katika mazingira mazuri, HAWOCODA
imewatambulisha rasmi wasaidizi hao wa Sheria katika sehemu zote husika za
kiserikali pamoja na kuwapatia vitendekea kazi vyote muhimu zikiwemo Katiba ya
Jamhuri ya muungano wa Tanzania na vijitabu vyote muhimu vya Sheria za nchi
vilivyoandikwa na kufafanuliwa kwa lugha nyepesi.
Mwisho
HAWOCODA inachukua fursa hii ya kuwashukuru wale wote walioshiriki katika kuanzisha
asasi hii, kwa namna moja au nyingine kwa kutumia muda wao, ujuzi pamoja na
fikra zao ili kuhakikisha asasi hii imesimama na kujitegemea. Wote kwa pamoja
wamechangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta karibu huduma ya Sheria kwa
wananchi wa kawaida wa Hanang na hasa wale ambao hawawezi kumudu kulipia huduma
muhimu za mawakili.

No comments:
Post a Comment