Powered By Blogger

Saturday, 4 March 2017

Hanang’ Women Counseling and Development Association


Hanang Women Counseling and Development Association (HAWOCODA) ni asasi isiyokuwa ya kiserikali ambayo ni ya kujitolea, inayojitegemea na ni asasi ambayo si ya kibiashara. Ilianzishwa mwaka 1992 na kusajiliwa rasmi mwaka 1994 chini wizara ya maendeleo ya jamii kwa nambari ya usajili SO.8263, ikiwa na lengo kuu la kutoa huduma za msaada wa Sheria kwa watu wote wasiojiweza waishio wilaya ya Hanang’ wakiwemo; watu maskini, wanawake, watoto, walemavu na watu waishio na virusi vya UKIMWI. Mbali na lengo hilo HAWOCODA pia imeanzishwa kwa madhumuni ya kueneza elimu ya Sheria kwa kuandika na kutoa machapisho mbalimbali ya Sheria. Hii ni moja ya njia za kuhakikisha kuwa wana Hanang wote wanapata elimu ya msingi inayohusiana na masuala ya Sheria hasa katika kujua haki zao ili kujenga jamii ambayo inaheshimu Utawala wa Sheria, Utawala Bora, na kuheshimu, kulinda, na kutekeleza misingi ya Haki za Binadamu.

Kazi za HAWOCODA

HAWOCODA inafanya kazi za Sheria zikiwemo; uwakilishi Mahakamani, na usuluhishi wa migogoro kwa kuzingatia maslahi ya watu maskini. Pia HAWOCODA inafanya kazi ya kutoa elimu ya Sheria kwa jamii ili kuongeza uelewa wa masuala ya Sheria na Haki za Binaadamu kwa kupitia semina, makongamano, midahalo na mijadala inayohusiana na masuala ya Sheria ili kuwawezesha watu kutoka sehemu tofauti kujadili sera za Sheria na kimaendeleo. HAWOCODA pia inaandaa mikutano ya kitaalamu kwa ajili ya kutoa mafunzo kutoka sekta tofauti katika jamii ya Hanang.

Shughuli za HAWOCODA
Malengo ya HAWOCODA yanatimizwa kwa kutekeleza shughuli zifuatazo:-

1. Ushauri wa Sheria;
2. Mafunzo ya Wasaidizi wa Sheria;
3. Mafunzo ya Haki za Binaadamu;
4. Utoaji wa Haki;
5. Usambazaji wa Majarida, Vitabu na Vipeperushi;

Dira ya HAWOCODA
Azma ya HAWOCODA ni kuhakikisha kwamba kila mwana Hanang, hasa watu maskini, wanawake, watoto, watu wenye ulemavu na makundi yote katika jamii wanaelewa vizuri haki zao za msingi za Sheria na kanuni za Haki za Binaadamu na pia waweze kuzidai ili kujenga jamii iliyojengwa kwenye msingi ya utawala wa Sheria, utawala bora na kuheshimu misingi ya haki za binaadamu.

Dhamira ya HAWOCODA
HAWOCODA imekusudia kuongeza uelewa wa jamii juu ya haki zao na wajibu kwa kutoa elimu ya Sheria na Haki za Binaadamu, utafiti wa maswala ya Sheria, kuendesha semina, warsha, mikutano, na kutoa ushauri wa msaada wa Sheria.

Wafanyakazi wa HAWOCODA
Kwa sasa HAWOCODA ina wafanyakazi na wahudumu wa kada mbali mbali wapatao 29 kutoka katika kata 11 za wilaya ya Hanang.

Maadili ya HAWOCODA
Watu wote wanaoshiriki katika shughuli za HAWOCODA ni lazima wawe ni watu wenye dhamira nzuri kwa watu wote katika masuala yote yanayohusiana na HAWOCODA, na hawaruhusiwi kutumia huduma pamoja na jina la HAWOCODA kwa ajili ya maslahi yao binafsi, kisaisa, kidini, kikabila, au jambo lolote ambalo liko nje ya malengo ya HAWOCODA.

Anwani
Unaweza kuwasiliana na HAWOCODA kwa anuani ifuatayo:-
Head Office (Katesh)
Hanang’ Women Counselling and Development Association (HAWOCODA)
S.L.P. 3, Katesh - Hanang.
Simu: +255 (0) 784 739 773 – Gidamis Shahanga (M/kiti wa Bodi)
          +255 (0) 784 779 096 – Mary Gitagno (Mratibu)
Ofisi ya Balang’dalalu:
Hanang’ Women Counselling and Development Association (HAWOCODA)
S.L.P. 3, Katesh - Hanang.
Simu: +255 (0) 686 209 304 – Christopher Digay
Barua Pepe: hawocoda@yahoo.com

Maelezo ya Jumla
Moja ya lengo kuu la HAWOCODA ni kutoa msaada wa Sheria bila ya malipo. Hivyo, kazi hii ilianza kutekelezwa mara tu baada ya kuanzishwa kwa HAWOCODA kwa kutumia wasaidizi wa Sheria waliopata elimu ya msingi ya Sheria mbalimbali za nchi na Katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Idadi ya watu wenye kuhitaji huduma hii ilikuwa ikiongezeka kila kukicha, na hivyo uhaba wa huduma hizo ulianza kuonekana. Baada ya kuongezeka kwa idadi ya watu wa Hanang na walio wengi kuanza kupata uelewa juu ya haki zao na hivyo kujitokeza kwa wingi kutaka huduma. Hapo ndipo HAWOCODA ilipoanza kutafuta njia mbadala ya kukidhi haja hiyo na kuona kuwa upo umuhimu wa kupanua wigo wa huduma za msaada wa Sheria mijini na vijijini. Hivyo basi HAWOCODA ilibuni utaratibu wa kuweka Wasaidizi wa Sheria katika sehemu zote za Hanang ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo.

Hivyo mnamo mwaka 2015 HAWOCODA ilianzisha rasmi mpango huo. Mpaka sasa, HAWOCODA imeweza kuwaajiri Wasaidizi wa Sheria wasiopunguwa 25 ambao wamesambazwa katika kata mbalimbali za wilaya ya Hanang. Wasaidizi hao wamepatiwa elimu ya msingi inayohusiana na masuala ya Sheria pamoja na kupata maelekezo kutoka kwa maafisa mipango wetu juu ya utoaji wa msaada wa Sheria.

Licha ya hayo HAWOCODA pia imeona iko haja ya kutayarishia Wasaidizi hawa muongozo ambao utakuwa unawaongoza katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi. Umuhimu wa muongozo huu ni kuwa umejaribu kugusia nyanja zote ambazo ni muhimu katika kuhakikisha Utawala wa Sheria unakuwepo wilayani ikiwemo; Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na misingi mikuu na kanuni muhimu zilizomo ndani yake kama vile Utawala wa Sheria, Uhuru wa Mahakama, Haki na wajibu wa Binaadamu, Utawala Bora, Mihimili mikuu ya Serikali pamoja na kazi zake, Sheria za ajira na mahusiano kazini, Sheria za Ardhi, Sheria za mwenendo wa Makosa ya Jinai na Makosa ya Madai, Sheria za Tawala za Mikoa, Sheria za mazingira, mikaaba ya kimataifa ya haki za wanawake, tamko la kimataifa la haki za binadamu, mkataba wa kimataifa wa kupinga aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake, na Sheria nyinginezo za nchi.

Katika kuhakikisha wasaidizi wa Sheria wanafanyakazi katika mazingira mazuri, HAWOCODA imewatambulisha rasmi wasaidizi hao wa Sheria katika sehemu zote husika za kiserikali pamoja na kuwapatia vitendekea kazi vyote muhimu zikiwemo Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania na vijitabu vyote muhimu vya Sheria za nchi vilivyoandikwa na kufafanuliwa kwa lugha nyepesi.

Mwisho HAWOCODA inachukua fursa hii ya kuwashukuru wale wote walioshiriki katika kuanzisha asasi hii, kwa namna moja au nyingine kwa kutumia muda wao, ujuzi pamoja na fikra zao ili kuhakikisha asasi hii imesimama na kujitegemea. Wote kwa pamoja wamechangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta karibu huduma ya Sheria kwa wananchi wa kawaida wa Hanang na hasa wale ambao hawawezi kumudu kulipia huduma muhimu za mawakili.